Nimekuwa nakutana na swali lifuatalo mara kwa mara, “Kuna tofauti gani ya saruji iliyoandikwa 32.5 na 42.5 ?
Saruji ni kichanganyishi kitumikacho kama gundi kwenye shughuli za ujenzi. Saruji inatokana na mchakato mrefu wa kiwandani kwa kutumia madini yachimbwayo toka ardhini.
Saruji inategemea na aina ya madini yanayochimbwa ardhini kwa maana kuna aina mbalimbali za madini na zenye sifa tofauti kulingana na mwamba wa eneo husika.
Kabla ya saruji kuwa saruji kamili yaani ukiiwekea maji inaganda, inachanganywa na kemikali ya kusababisha igande. Ndo maana kama mkandarasi akigundua kuna wizi sana katika eneo la mradi basi hii kemikali huwekwa wakati wa kufanyia kazi.
Saruji hutengenezwa ikiwa inatofautiana kutokana na matumizi husika, kuna saruji ya miradi ya kwenye madaraja ya mito isiyokauka maji, baharini, kwenye maziwa, sehemu zenye chumvi sana n.k. Ili kutofautisha aina hizi za saruji maandishi huwekwa kwenye mifuko iliyobeba saruji, na kwetu hapa mifuko hii huwa na uzito wa 50kg na ujazo wa 0.0345m³ ambapo tani moja huwa mifuko 20 na 1m³ huwa mifuko 29.
Ukiangalia mifuko ya saruji utaona 32.5 au 42.5 hizi namba zina maana kubwa katika kuitambulisha hiyo saruji, namba hizi husimama kuwakilisha uimara wa saruji husika, ukiona namba kubwa inamaanisha saruji hiyo ni imara kulinganisha na namba ndogo. Mfano 42.5 ni imara zaidi kuliko 32.5 yaani ukiita wahandisi wenye nyundo za kupimia zege kwa siku zinazolingana utakuta ile yenye 42.5 ina kipimo kikubwa ukilinganisha na 32.5 .
Si hivyo tu hizi namba zinaenda hadi 62.5 ,pia huambatana na herufi baada ya namba mfano 32.5N au 32.5R au 42.5L,hizi herufi ni vifupisho vya maneno ya kiingereza zikimaanisha:
N = Normal
R = Rapid
L = Low
Kwa kifupi R zikimaanisha saruji hiyo hukauka haraka
L saruji hii hukauka taratibu sana
N saruji hii hukauka kawaida
32.5L 42.5L 52.5L 62.5L
32.5N 42.5N 52.5N 62.5N
32.5R 42.5R 52.5R 62.5R
Baada ya siku 28 uimara wa saruji zote huwa sawa, hizo namba zimewekwa ili kurahisisha kazi kwa matumizi mbalimbali pia kuwa na spiidi ya kazi katika ujenzi. Mfano Kama unataka kutoa formwork haraka ili uanze kujenga tofali basi unatumia namba husika.